MKAZI wa Iringa
Mjini, Ramadhan Mrisho (Makosa), ametangaza kuuza figo yake moja kwa kile
anachodai anatafuta fedha za kumsaidia kuendesha maisha yake.
Akizungumza na
gazeti hili hivi karibuni mjini Iringa, Mrisho, alisema amefikia uamuzi wa
kutangaza kuuza figo yake akiwa na akili timamu.
“Nisidhaniwe nimekuwa na akili tofauti,” alisema Mrisho na kuongeza;
“Nina akili timamu, nimeamua kuchukua uamuzi huu kama nilivyosema kwa lengo la
kujikwamua kiuchumi.”
Hata hivyo Mrisho hakuwa tayari kutaja bei ya figo yake iwapo atapatikana
mteja. Alisema anajua wapo watu wenye matatizo ya figo na wamekuwa wakisafiri
mbali na nchi kutafuta tiba.
“Kama kuna mtu ana matatizo ya figo au ameitafuta ameikosa aje kwangu
tukubaliane bei,” alisema Mrisho.
Katika harakati zake za kutafuta fedha za kusaidia familia yake, Julai, 2012
Mrisho alitishia kujinyonga, tukio alilopanga lifanyike Uwanja wa Samora kwa
sharti kuwa mashuhuda kutalipa kiingilio ambacho kingekusanywa kwa ajili ya
familia yake.
Wakati huo huo, Mrisho alinukuliwa akisema kuliko familia yake kuendelea
kutaabika ni bora ajitoe mhanga ili fedha zitakazopatikana kama kiingilio
zitumike kusaidia watoto yake.
Hata hivyo, alisema mpango wake haukufanikiwa kwani akiwa kwenye maandalizi
walitokea watu mbalimbali wakiwemo Polisi waliompa ushauri nasaha, hivyo
alisitisha mpango huo.
“Sasa nimekuja na mpango mpya, mpango huu si mwingine zaidi ya huu wa kuuza
figo yangu moja, naamini nikifanikiwa nitapata fedha,” alisema.
Mrisho ambaye ni maarufu mkoani Iringa kutokana biashara zake zake nyingi
alizokuwa akifanya mwanzoni mwa miaka ya tisini baada ya kuacha kazi yake ya
ubaharia.
Wakati akifika mjini Iringa, Mrisho alikuwa hanywi pombe, bali alikuwa
mnyenyekevu ambapo alijikita kuisaidia jamii ya watu wa Iringa kutunza mazingira
kwa kupanda miti kila mtaa.
Aliongoza kupanda miti ya aina mbalimbali ikiwemo ya matunda inayoonekana mjini
Iringa.
Mrisho ndiye alikuwa mtu wa kwanza mjini Iringa kuingiza mabasi madogo ya
kusafirisha abiria aina ya Coaster yaliyokuwa yakifanya kazi katika maeneo
mbalimbali ya mjini Iringa.
Pamoja na biashara ya usafirishaji, Mrisho alijikita katika biashara ya hoteli.
Na kwa muda mrefu aliendesha hoteli ya CATS iliyopo jirani na Maktaba ya Mkoa
wa Iringa.
Kwa kadri biashara ilivyozidi kumchanganyia katika hoteli hiyo, alimua
kuibadili jina na kuiita MAKOSA CATS Hotel.
Katika hoteli hiyo bendi nyingi zimepiga muziki na kwa mara ya mwisho,
mwanamuziki Macay Fanta alikuwa akifanya shoo zake mpaka pale Mrisho
aliposhindwa kuiendesha mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Mtandao wa biashara za Mrisho haukuishia hapo, alikuwa pia akimiliki hospitali
maarufu sana iliyopo jirani kabisa na Soko Kuu la Mjini Iringa, ambayo ilikuwa
ikiitwa MAKOSA.
Alisema biashara zote hizo haziko tena mikononi mwake na ugumu wa maisha
unazidi kumwandama. Alisema anatafuta njia za kujikwamua na njia halali
anayoiona mbele yake hivi sasa ni kuuza figo yake moja.
Chanzo:Majira