Geita/Dar. Mama wa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ambaye alitekwa juzi na watu wasiofahamika mkoani Geita, amefanyiwa upasuaji wa kichwa na jopo la madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) mjini Mwanza.
Mama huyo aliyefahamika kwa jina la Ester Jonas
(30), alilazimika kufanyiwa upasuaji huo baada ya kushambuliwa kwa
kukatwa mapanga na watu hao ambao walimteka mtoto wake juzi akiwa
amembeba mgongoni nyumbani kwake.
Mkuu wa Kitengo cha dharura cha Hospitali ya
Bugando, Dk Darick David alisema mama huyo alifikishwa hapo jana akiwa
na hali mbaya kutokana na kuvuja damu nyingi.
“Namkumbuka mwanangu Yohana Bahati,” hayo ni
maneno aliyoyasema mama mzazi wa mtoto huyo akiwa hospitalini hapa
kwenye chumba namba 903 cha uangalizi maalumu (ICU).
“Kama mnavyomuona hali yake siyo nzuri, hata
kuzungumza hawezi, alikatwa panga kichwani jeraha kubwa liko puani,
tumelazimika kumfanyia upasuaji wa kichwa ili kusafisha damu iliyokuwa
imeganda ndani,” alisema Dk David na kuongeza: “Bado anatatizo kubwa na
madaktari bingwa wanaendelea kumchunguza.”
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Profesa Alfred
Mteta alisema: “Inasikitisha kuona binadamu unamfanyia unyama binadamu
mwenzako, kamwe vitendo hivi haviwezi kukubalika tumempokea mgonjwa huyu
na madaktari wanaendelea kumpatia matibabu ili kuokoa maisha yake.”
Mbunge Viti Maalumu
Mbunge wa Viti Maalumu anayewawakilisha watu wenye
ulemavu wa ngozi bungeni, Al-Shaymaa Kwegyir ametaka nguvu zinazotumiwa
na polisi kuwakamata majambazi, zitumike pia kuwasaka wanaoteka na
kuwaua watu wenye ulemavu huo.
Kauli ya Kwegyir imekuja baada ya kuanza kuibuka
kwa matukio ya utekaji na kuwaua wenye ulemavu wa ngozi kwa imani za
kishirikina.
Hivi karibuni, mtoto mwingine mwenye ulemavu wa ngozi mkoani
Geita alitekwa na mama yake kucharangwa mapanga. Utekaji huo umetokea
ikiwa ni siku 50 sasa tangu kutoroshwa kwa mtoto, Yohana mkoani Mwanza.
“Polisi wana nguvu za kukamata majambazi, kwanini
nguvu hiyo isitumike kuwabaini wanaojihusisha na vitendo hivi, tumeanza
kuwa na shaka juu ya utendaji kazi wao kuwa unaegemea upande fulani,”
alisema Kwegyir.
Alisema kuna haja ya serikali na polisi kuongeza jitihada ili kumaliza tatizo hilo linaloonekana kushamiri kwa kasi.
“Nilikuwa Nyakato mwezi uliopita, kuna mtoto wa
miaka minne alinusurika kunyakuliwa na watu waliokuwa kwenye pikipiki,
kwa bahati nzuri mama yake alimuwahi, matukio kama haya yanaashiria kuwa
hali ni mbaya,” alisema.
Barwany alia na mfumo
Akizungumzia matukio hayo, Mbunge wa Lindi Mjini
(CUF), Salum Barwany ambaye pia ana ulemavu wa ngozi, alidai kutopatiwa
ufumbuzi kwa tatizo hilo la utekaji na mauaji ya watu wenye ulemavu wa
ngozi kunaashiria kuwa wahusika wakuu wa vitendo hivyo huenda
wanafahamika hivyo kuna baadhi ya watu wameamua kuwalinda.
Barwany alisema inashangaza kuona Serikali
ikishindwa kulipatia uzito suala hilo kwa kuendelea kuwaacha wahusika
wakiendeleza unyama wao.
“Ni jambo la aibu kwa Serikali kushindwa kuchukua
hatua, tumeshapiga sana kelele mpaka inafikia hatua tumeamua kumwachia
Mungu maana nguvu inapelekwa kwa waganga wa kienyeji, lakini ukweli ni
kwamba kuna watu nyuma yao,” alisema Barwany na kuongeza;
“Nashangaa mambo haya yanavyoshika kasi wakati huu
wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu na kama mwelekeo ndiyo huu, basi
tusubiri matukio mengi zaidi ya haya.”
Alifafanua kuwa viongozi wengi wa Serikali
wamekuwa wakipiga kelele pale tukio linapotokea, baada ya hapo hakuna
ufuatiliaji unaoendelea.
Alisema kuthibitisha hilo, hata Bunge mara kadhaa
limeshindwa kujadili suala hilo kwa madai kuwa kuna mambo mengine yenye
umuhimu zaidi licha ya kutambua kuwa maisha ya walemavu hao yanazidi
kuwa hatarini.
Itakumbukwa, Januari 29, 2009, Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda alimwaga chozi bungeni mjini Dodoma kuonyesha uchungu
aliokuwa nao dhidi ya mauaji ya albino yaliyokuwa yameshamiri nchini.
Alitamka wazi kuwa ‘wanaoua albino nao wauawe’.
Maalbino Geita
Chama cha Watu wenye Ulemavu wa Ngoz (Tas) mkoani
Geita, kimeyahusiha matukio ya mauji hayo na Uchaguzi Mkuu huku baadhi
ya wanasiasa wakitajwa kuhusika.
Kaimu Mwenyekiti wa Tas Mkoa wa Geita, Isaack
Timothy akizungumza juzi baada ya tukio la mtoto Yohana Bahati(1)
kutekwa Februari 15 saa 2 usiku, alisema suala hilo ni la wazi kwa kila
Mtanzania ambaye akitafakari kwa makini anaweza kubaini hivyo.
Makachero kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, wamewasili Geita kuwasaka washukiwa wa utekaji wa mtoto Yohana.
Mtoto huyo mkazi wa kijiji cha Ilelema wilayani
Chato mkoani Geita, alitekwa na watu wasiojulikana wakiwa wawili ambao
walivamia nyumbani kwa wazazi wake na kumjeruhi mama yake.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo
alithibitisha kuwasili kwa makachero hao ambao wanaungana na wa Geita
kuhakikisha mtoto huyo anapatikana.
“Pia tunashirikiana vya kutosha na askari wa mikoa
mingine...na wananchi tunaomba watuunge mkono, wakiona kuna mtu
wanamtilia shaka labda kwa kuomba maji, au kuuliza njia watoe
taarifa…kuna polisi jamii huko. Kila kata na tarafa kuna polisi
washirikiane na hao askari,” alisema Konyo.
Konyo alisema familia hiyo, ilikuwa na watoto
watatu wenye ulemavu wa ngozi ambao ni pamoja na Shida (11) na Tabu (3)
ambao kwa sasa wanahifadhiwa na Serikali ya Wilaya ya Geita.
No comments:
Post a Comment