RAIS
Jakaya Kikwete amesema kamwe Tanzania haitatumia nguvu kumaliza mvutano
kati yake na Malawi kuhusu mpaka kati ya nchi hizo, huku akiongeza
kuwa, Tanzania haioni mantiki ama busara yoyote kuingia vitani na nchi
yoyote jirani kwa sababu yoyote ile.
Alitoa
uhakikisho huo kwa Malawi na nchi nyingine jirani wakati alipohutubia
mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia kwa mamia ya wananchi kwenye
Uwanja wa Michezo wa mjini Mbamba Bay, Mji mkuu wa Wilaya mpya ya Nyasa,
juzi. Mji huo uko kwenye pwani ya Ziwa Nyasa.
Rais Kikwete ambaye alikuwa anasemea juhudi za kutafuta ufumbuzi wa suala la mpaka kati ya Tanzania na Malawi, alisema: “Nataka
kuwatoeni wasiwasi. Hakuna sababu ya vita.Laleni usingizi bila
wasiwasi, kuleni samaki wenu kwa sababu Tanzania haioni busara ya vita.”
“Tanzania
haiwezi kutumia nguvu kupata suluhisho la mvutano wa mpaka. Tuna uwezo
wa kupata jawabu la tatizo hilo bila kutumia njia ya vita. Tanzania
haioni busara hiyo ya vita. Tuna uwezo wa kupata ufumbuzi kwa njia ya
majadiliano. Na wala msimamo huo siyo kwa mpaka wetu na Malawi pekee
bali kwa mipaka yote ya Tanzania,” alisema Rais Kikwete.
Rais
Kikwete pia ameelezea juhudi ambazo zimekuwa zinafanywa na Tanzania
kutatua tatizo hilo la mpaka ikiwa ni pamoja na kuliomba jopo la Marais
wastaafu kusaidia kutafuta jawabu la mpaka kati ya nchi hizo mbili.
Marais
hao Joachim Chissano wa Msumbiji, Festus Mogae wa Botswana na Thabo
Mbeki wa Afrika Kusini wanasaidiwa na jopo la Kimataifa la mabingwa wa
Sheria katika kazi yao hiyo.
Rais
pia amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Nyasa kuwa ahadi na mpango wa
Serikali kununua na kuweka meli mpya katika Ziwa Nyasa uko pale pale na
kwamba mipango inafanywa ya kuhamisha chelezo cha kujengea meli kutoka
Mwanza kwenye Ziwa Victoria kuipeleka Itungi, Kyela, Mbeya ili kuanza
ujenzi wa meli hiyo.
Rais
ambaye katika Kampeni ya Uchaguzi Mkuu Mwaka 2010 aliahidi ununuzi wa
meli tatu za kutoa huduma katika maziwa makuu ya Tanzania ya Victoria,
Tanganyika na Nyasa amesema kuwa kiasi cha Sh bilioni 23 zimetengwa
tayari kwa ajili ya kuanza ujenzi wa meli hiyo.
Amesema
kuwa michoro ya meli hiyo ya Ziwa Nyasa imelazimika kubadilishwa kidogo
kwa sababu ya ukweli kuwa ziwa hilo lina mawimbi makali na huchafuka
mara kwa mara tofauti na maziwa Victoria na Tanganyika.
Rais
Kikwete pia amewaambia wananchi kuwa Serikali inaendelea na mipango ya
kujenga reli kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay ili kuzidi kufungua ukanda wa
Mtwara na kuweza kubeba chuma na makaa ya mawe kutoka Liganga na
Mchuchuma, maeneo yaliyoko katika Mkoa wa jirani wa Njombe na wilaya
jirani za Nyasa na Ludewa katika Mkoa huo wa Njombe.
Kabla
ya kuhutubia mkutano wa hadhara, Rais Kikwete ambaye alikuwa katika
siku ya pili ya ziara yake ya siku sita katika Mkoa wa Ruvuma, Rais
Kikwete alikuwa na shughuli nyingi katika Wilaya ya Nyasa ambako
amezindua Daraja la Ruhekei lililoko katika Kijiji cha Mkalole, kilomita
nane kutoka mjini Mbamba Bay.
Alisema
ujenzi wa daraja hilo ambalo lina sehemu tatu limejengwa kisasa kabisa
ikiwa ni maandalizi ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbinga, Wilaya
ya Mbinga kwenda Mbamba Bay, Wilaya ya Nyasa.
“Ni
kweli Mwaka 2005 wakati wa kampeni ya Uchaguzi Mkuu nilishindwa kuvuka
hapa kwa sababu daraja lilivunjika lakini ujenzi huu wa kisasa ni kwa
sababu tunajiandaa kujenga barabara ya lami kuunganisha Mbinga na Mbamba
Bay,” Rais Kikwete amewaambia wananchi kwenye daraja hilo.
Rais
Kikwete pia ameweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Makao Makuu ya Wilaya
ya Nyasa katika Kijiji cha Kilosa kilichoko karibu na Mbamba Bay na
amezindua usambazaji wa umeme katika vijiji vya Wilaya ya Nyasa. Rais
Kikwete anaendelea na ziara yake mkoani Ruvuma.