Nyasa. Safari ya mwisho ya mbunge wa Mbinga
Magharibi jana ilihitimishwa saa 9.25 alasiri wakati mwili wake
ulipofunikwa na mfuniko mkubwa wa zege uliobebwa na gari maarufu kwa
jina la “kijiko”.
Haikuwa kitu cha kawaida wakati gari hilo kubwa
likishusha mfuniko huo wa zege kwenye kaburi la mwimbaji huyo maarufu wa
nyimbo za uhamasishaji za CCM na kiongozi wa kundi la Tanzania One
Theatre (TOT), lakini majonzi yaliwafanya waombolezaji kulichukulia
tukio hilo kuwa la kawaida.
Safari ya Komba, iliyoanza miaka 61 iliyopita
kwenye kijiji cha Lituhi ambako aliazikwa jana, ilikamilishwa kwa salamu
mbalimbali ambazo zilielezea ushupavu wa kapteni huyo mstaafu wa jeshi.
Mazishi hayo yaliyohudhuriwa na mamia ya wananchi,
wakiwamo viongozi mbalimbaliwakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete na mkewe
Salma, yalifanyika katika makaburi ya Misheni,katika Kijiji cha Lituhi
(Bundi) wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
Nyuso za majonzi zilitawala kwa waombolezaji
waliojitokeza nyumbani kwa marehemu, takriban mita 500 kutoka katika
makaburi hayo na baadaye katika misa iliyofanyika kwenye uwanja wa Shule
ya Msingi ya Lituhi, ikiongozwa na Askofu John Ndimbo wa Jimbo Katoliki
la Mbinga.
Kaimu katibu wa Bunge, John Joel, akisoma wasifu
wa marehemu, alisema Kapteni Komba aliyefariki dunia Februari 28, mwaka
huu akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam,
alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya shinikizo la damu na mara kadhaa
Ofisi ya Bunge ilimpeleka India kwa matibabu. Pia alikuwa na tatizo la
kisukari ambalo ndilo lililochukua maisha yake.
Mazishi hayo yalishuhudiwa na viongozi mbalimbali,
akiwamo Edward Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu, Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, Steven Wasira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Utaratibu na Bunge), Jenister Mhagama na mbunge wa Songea Mjini,
Dk Emmanuel Nchimbi.
Wengine ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete,
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Ali Abdallah Ali, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Spika wa Bunge,
Anne Makinda.
Uwanja wa ndege
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Songea, viongozi
mbalimbali waliwasili kwa ndege za kukodi na Lowassa ndiye aliyefungua
mlango kwa ndege iliyotua saa 2:33 asubuhi akiambatana na mbunge wa
Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani.
Haikupita muda mrefu, ndege nyingine ilitua saa
2:50 ikiwa na Spika Makinda na msafara wake uliomjumuisha mbunge wa
Ludewa, Deo Filikunjombe.
Saa 3:22 ilitua ndege iliyobeba ujumbe wa CCM
ukiongozwa na Kinana. Wengine waliokuwamo ni naibu katibu mkuu ambaye
pia ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, katibu wa itikadi na
uenezi, Nape Nnauye na mwimbaji wa kikundi cha TOT, Khadija Kopa. Pia
baadaye Rais Kikwete alitua na ndege ya Serikali.
Mwili wa marehemu uliwasili ukiwa katika moja ya ndege mbili zilizobeba familia yake, ndugu na watu mbalimbali wa karibu.
Fulana za Lowassa
Wakati ibada ya misa ikiendelea, walionekana
vijana wakiwa wamevaa fulana nyeupe na nyeusi zenye ujumbe wa “Marafiki
wa Lowassa”, zilizokuwa zimeandikwa mbele “4 U Movement Lowassa” huku
mgongoni zikiandikwa “Kapteni John Damiano Komba 1954-2015 Friends of
Lowasa”.
Baada ya vijana hao kuonekana, mmoja wa viongozi
wa Bunge alimwamuru mmoja wao aliyekuwa anapiga picha kwenda kuivua,
lakini aligoma na hakuna kati yao aliyekubali kuivua hadi mazishi
yalipomalizika. Mmoja wa vijana hao ambaye aligoma kutaja jina lake
aliiambia Mwnanchi akisema: “Kwa sasa fulana zimeisha kwa kuwa
zilizokuwa zinagawiwa. Lakini kama unazitaka unaweza kuacha namba yako
na utaletewa sehemu yoyote utakapokuwa.
“Tumeamua kutoa fulani hizi kama zawadi ya
kumbukumbu kwa mchango alioutoa Komba wakati wa urafiki wao (na Lowassa)
na ndiyo maana unaona tumezivaa.”
Salamu za rambirambi
Katika salamu zake, Gasper Tumaini, katibu wa
kikundi cha Sanaa cha TOT kilichokuwa kikiongoza Kapteni Komba, alisema
Komba alipenda jimbo lake na chama chake na kuwa siku moja kabla kifo
walikwenda kurekodi nyimbo za uchaguzi. Kwa niaba ya Kambi ya Upinzani,
mbunge wa Lindi Mjini (CUF), Salum Barwany alisema: “Tunatoa pole kwa
wananchi na familia kwa kuondokewa na mbunge mahiri na shupavu, tumefika
kuonyesha namna Komba alivyoishi vizuri nasi.
“Kila mmoja amejifunza namna Komba alivyoishi na
watu vizuri , alikuwa akinipa faraja wakati matukio ya mauaji ya albino
yalipotokea na wakati wote alikuwa akinihakikishia usalama wangu, hivyo
tumepata pigo kubwa kwa kuondoka kwake.”
Katibu Mkuu CCM, Abdulahman Kinana, alisema: “Tuna
huzuni kubwa kutokana na msiba mkubwa uliotokea. Komba alifanya kazi
nzuri ya kuwahudumia na kuwajali na kuangalia maslahi ya wananchi
aliowaongoza. Alhamisi iliyopita alikuja ofisini kwangu na kuniambia
anakwenda kiwandani kutafuta mabati 900 kupeleka jimboni kwake.”
Waziri Mhagama kwa niaba ya Serikali alisema:
“Komba alikuwa kiungo muhimu kwa serikali. Wengi wamemzoea katika
masuala ya siasa na chama, wote wanamkumbuka kwa tukio la kuimba nyimbo
za maombolezi wakati wa msiba wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.”
Spika Makinda alitumia fursa hiyo kuzungumzia
muswada wa mabadiliko katika sheria za Kiislamu ya mwaka 1963 kuhusu
Mahakama ya Kadhi akisema inatakiwa kubadilishwa kushughulikia mirathi,
talaka hivyo Wakristo wawe wavumilivu, wasikubali kuzungumzia vitu
ambavyo hawana uhakika navyo.
source Mwananchi
source Mwananchi
No comments:
Post a Comment