Thursday, March 12, 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Amina Masenza kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea tarehe 11 Machi, 2015 Mafinga katika Mkoa wa Iringa katika eneo lijulikanalo kwa jina la Changarawe, ambayo imepoteza uhai wa watu zaidi ya 40 waliokuwa wakisafiri kwa basi hilo na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Ajali hiyo imetokea baada ya basi la Kampuni ya Majinja Express walilokuwa wakisafiria watu hao kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam kugongana na lori lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mbeya, hivyo kusababisha kontena lililokuwa limebebwa na lori hilo kuliangukia basi.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kufuatia taarifa za vifo vya watu zaidi ya 40 huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika ajali hii mbaya ambayo imesababisha simanzi na majonzi makubwa kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu”, amesema Rais Kikwete akiomboleza msiba huu.
“Huu ni msiba mkubwa, na Taifa kwa ujumla limepata pigo kubwa, hivyo naomba upokee salamu zangu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kutokana na ajali hii iliyotokea Mkoani kwako. Naomba, kupitia kwako, rambirambi zangu na pole nyingi ziwafikie watu wote waliopotelewa ghafla na wapendwa wao. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Roho za Marehemu wote mahala pema peponi, Amina”, ameongeza kusema Rais Kikwete.
Katika Salamu zake hizo, Rais Kikwete amewahakikishia wafiwa wote kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba wa ndugu na jamaa zao, lakini amesema, pamoja na machungu yote ya kupotelewa na ndugu na jamaa zao, anawaomba wafiwa wawe na moyo wa uvumilivu na subira wakati huu wanapoomboleza vifo vya wapendwa wao.
Aidha, Rais Kikwete amehitimisha rambirambi zake kwa kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema watu wote waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo wapone haraka, ili waweze kuungana tena na ndugu na jamaa zao.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
11 Machi, 2015

No comments:

Post a Comment

Popular Posts