TAARIFA
KWA UMMA KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA DENGUE “DENGUE FEVER”
Utangulizi
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa
taarifa kwa Umma juu ya mwenendo wa ugonjwa wa homa ya dengue yaani “dengue
fever” hapa nchini.Ugonjwa huu umethibitishwabaada ya sampuli
zilizochukuliwa kutoka kwa watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huu jijini Dar es
Salaam kupelekwa kwenye maabara yetu ya Taifa Dar es salaam na kuthibitisha
kuwa na virusi vya homa ya dengue mnamo mwishoni mwa mwezi wa Januari 2014.
Hadi sasa idadi ya wagonjwa ambao wamethibishwa kuwa na ugonjwa huuni 400 na
Vifo 3. Kwa wiki iliyoshia tarehe 9 Mei 2014 ya idadi ya wagonjwa
waliogundulika mkoani Dar es salaam ni 60 (42-Kinondoni, 14-Temeke na 4-Ilala)
na idadi ya wagonjwa waliopo wodini mpaka sasa ni 13.
Aidha, mlipuko wa ugonjwa huu si mpya hapa nchini
kwani uligundulika kwa
mara ya kwanza mnamo
Juni 2010 mkoani Dar es Salaam ambapo idadi ya watu 40 walithibitika kuwa na
ugonjwa. Pia, kati ya mwezi Mei hadi Julai 2013,wagonjwa 172 walithibitishwa
kuugua ugonjwa huu.
Homa ya Dengue
Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi
ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes.
Dengue in ugonjwa uliosambaa duniani katika nchi za
ukanda wa joto. Takribani asilimia 40 ya watu wote duniani wanaishi katika nchi
zenye ugonjwa huu. Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinathibitisha kuwa
takribani matukio milioni 5 ya Dengue yanatolewa taarifa kila mwaka. Watu laki
5 hulazwa hospitali kwa kuathirika na Dengue kali. Homa ya Dengue imeshatokea
katika nchi zipatazo 34 barani Afrika.
Hapa Afrika Dengue ni ugonjwa unaojulikana kwa kiwango
kidogo sana. Licha ya kwamba milipuko ya kwanza imetokea tangu mwanzoni wa
karne ya 19. Matukio ya Ugonjwa huu yameongezeka Afrika tangu miaka ya 1980,
matukio mengi yakitokea nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika ikiwa ni pamoja
na Msumbiji, Somalia, Kenya, Komoro, Djibouti na Tanzania. Ikumbukwe kuwa jina
“Dengue” linatokana na neno “Dinga” la kiswahili linalolomaanisha ugonjwa
unaotakana na pepo yaani Kudinga pepo. Mabaharia wa Kispanish walipokuja kwenye
pwani ya Afrika Mashariki walirudi kwao na kuuita “Dengue”.
Dalili za ugonjwa huu ni homa, kuumwa kichwa, maumivu
ya viungo na uchovu Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia
katisiku ya 3 na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya dengue. Kwa
wakati mwinginedalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za
malaria, hivyo basi wananchi wanaombwa kuwa wakati wakipata homa kuhakikisha
wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria ua la ili hatua stahiki
zichukuliwe.
Kuna aina 3 tofauti za namna ugonjwa huu unavyoweza
kujitokeza iwapo mtu aking`atwa na mbu mwenye virusi hivi;
i.Homa ya dengue (Dengue Febrile Illness): Aina hii huambatanana dalili kuu tatu za homa kali ya ghafla, kuumwa
kichwa na maumivu ya viungo au uchovu.Aidha, kwa Tanzania mpaka sasa
zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wamejitokeza na dalili hizi.
ii.Dengue ya damu (Dengue Haemorrhagic Fever):
Aina hii yahoma ya dengue huambatana na dalili za mgonjwa kutokwa na damu
kwenye fizi au puani, vile vile kutokwa na damu chini ya ngozi.Iwapo mgonjwa
huyu ataumia sehemu yoyote ni rahisi kwake kupoteza damu nyingi kupitia kwenye
michubuko.
iii.Dengue ya kupoteza fahamu (Dengue Shock
syndrome): Aina hii ya homa yadengue huambatana na mgonjwa kupoteza damu
nyingi ambayo hupelekea mgonjwakupoteza fahamu. Dalili hizi zimeonekana kwa
mgonjwa 1 kati ya wagonjwa 400 waliokwisha kuthibitishwa kuwa na ugonjwa hapa
nchini.
Kirusi cha homa ya Dengue kinaambukizwa kutoka mtu
mmoja hadi mwingine kwa kuumwa na mbu wa Jamii ya Aedes, na
hasa Aedes aegypti. Mbu huyu anaishi katika mazingira ya makazi ya
binadamu. Huuma wakati ya mchana ndani ya nyumba au kwenye maeneo yenye vivuli,
hususani majira ya asubuhi na jioni kabla jua halijazama.
Mbu huyu anazaliana katika maji yaliyotuama hasa
kwenye vyombo vya nyumbani, makinga maji ya paa za nyumba, matairi ya gari,
ndoo, vikopo, na kadhalika. Kwa bahati mbaya mbu huyu huweza kuzaliana katika
vifaa vidogo vidogo ambavyo watu wengi huvidharau. Hivi ni pamoja na makopo ya
kuotesha maua, vikombe, vifuu vya nazi, na kadhalika. Majani mapana
yanayohifadhi maji ni mazingira mazuri kwa kuzaliana kwa mbu huyu, hivyo maeneo
ya bustani siyo ajabu kuwa mahali pazuri kwa mbu hawa.
Ugonjwa huu hauambukizi kwa kumhudumia mgonjwa au
kugusa majimaji yanayotoka kwa mgonjwa. Homa ya dengue inaweza kutibika kama
mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka.Hakuna
dawa maalumu ya ugonjwa wala chanjo bali mgonjwa anatibiwa kutokana nadalili
zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji au damu. Endapo
mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu, mgonjwa anaweza kupoteza maisha.
Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa
homa ya dengue
Kuangamiza mazalio ya mbu
- Fukia madimbwi ya maji yaliyotuamaau
nyunyuzia viuatilifu vya kuua viluwiluwivya mbu kwenye
madimbwi hayo
- Ondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya
mbu kama vile: vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa
hovyo, nk.
- Fyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu
- Hakikisha maua yandayopandwa kwenye makopo au
ndoo hayaruhusu maji kutuama
- Funika mashimo ya maji takakwa mfuniko imara
- üSafisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu
maji kutuama
Kujikinga na kuumwa na mbu
- Tumia viuatilifu vya kufukuza
mbu “mosquito repellants”
- Vaa nguo ndefu kujikinga na kuumwa na mbu
- Tumia vyandarua vilivyosindikwa viuatilifu (kwa
wale wanaolala majira ya mchana na hasa kwa watoto)
- Weka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba
za kuishi
Hatua zinazochukuliwa na Wizara
(i)Hatua za Dharura
Uratibu
- Timu ya Taifa ya Maafa inayoshirikisha wadau
mbalimbali ikiwemo wa Halmashauri za Jiji na Wadau wa Maendeleo hukutana
kila mara 2 kwa wiki kutathmini mikakati ya dharura iliyowekwa.
Uelemishaji na
Uhamasishaji wa Jamii
- Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilitoa tamko la
Serikali kwa nyakati tofauti kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Dengue. Tamko la
kwanza lilitolewa kwenye vyombo vya habari tarehe 04 Februari 2014 na
Machi 2014.
- Kuendelea kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa
huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara.
Aidha taarifa hii pia iinajumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa
(Ainisho la Ugonjwa), “Ukweli Kuhusu Ugonjwa“(Fact sheet), Mwongozo kwa
watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli. Vipeperushi vinavyoelezea
jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu vitatolewa.
- Kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia Radio,
na Runinga. Aidha Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za jiji
wameendelea kutumia Maafisa Afyaikiwemo wa kata kuwaelemisha wananchi
namna ya kudhibiti ugonjwa kwakutumia vipaza sauti, uongozi wa mitaa
Mafunzo kwa watalaam wa Afya
- Kuendelea kutoa elimu ya Afya kwa Watumishi wa
Afya ikiwa pamoja na madaktari na mafundi maabara namna ya kutambua
ugonjwa huu. Aidha watumishi wa hospitali za Muhimbili, Mwananyamala,
Amana na Temeke wamekwisha kupewa mafunzo haya na bado wanaendelea kupewa
kupitia mikutano yao ya asubuhi (Clinical meetings). Mafunzo haya pia
yanaendelea kutolewa kwa vituo vya chini kupitia Halmashauri
Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji
na mawasiliano
- Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika
vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na mipakani kupitia mfumo wa
saveilensi ya Wizara. Aidha, pamoja na Mwongozo huu, Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii imetoa maelekezo kwa Waganga wakuu wa mikoa na wilaya hapa
nchini kutoa taarifa za wagonjwa wa Dengue Fever kupitia taarifa za kila
juma.
- Kutoa miongozo ya ufuatiliaji wa ugonjwa huu
katika maeneo ya mipakani kuhusu kutokuwepo kwa aina yoyote ya vikwazo
vitakavyowekwa kwa ajili kwa wasafiri. Aidha maelekezo hayo yameainisha
kuwa iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na dalili tajwa atoe
taarifa kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahili ziweze
kuchukuliwa
- Kufuatilia kwa karibu ongezeko la wagonjwa wenye
homa isiyo kuwa ya malaria kwa Mikoa na Wilaya zote nchini ili kuweza kufanya
uchunguzi wa kina iwapo kuna ugonjwa huu. Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii imeshafanya utafiti mkoani Kagera, Morogoro na Kigoma na
kuthibitisha kuwa haijaadhirika na dengue.
- Kuanzishwa kwa vituo maalum vya ufuatiliaji wa
ugonjwa huu katika Hospitali za Manispaa za jiji la Dar es Salaam
(Mwananyamala, Amana na Temeke). Aidha, Kituo cha ‘International School of
Tanganyika – IST’ kilichopo Manispaa ya Kinondoni na Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili zinaendelea na ufuatiliaji wa ugonjwa huu. Aidha Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii itafungua pia vituo mkoani Tanga na Mtwara, mikoa
imayopakana na nchi jirani yaani Kenya na Msumbiji ambako ugonjwa huu pia
umetolewa taarifa.
- ·Kupeleka taarifa
ya mlipuko huu Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kama mwongozo wa Kanuni
za Afya za Kimataifa uvyaoelekeza.
Upimaji na Tiba
- Kuimarisha uwezo wa kutambua ugonjwa huu kwa kina
kupitia maabara ya Taifa (NHLQATC) iliyopo NIMR. Vile vile Wizara
imepeleka vipimo sawia yaani “Dengue Rapid Test Kits” kwa vituo vya Dar es
Salaam kuimarisha utambuzi. Vituo hivo ni pamoja na hospitali za
Muhimbili, Amana, Mwananyamala, Temeke Hospital, na IST kliniki. Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii imeagiza Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuhakikisha
vitendanishi hivi vinakuwepo ili kurahisisha upatikanaji wake kwa
Halmashauri zote na kupelekwa kwenye vituo vya chini zaidi. Wizara
imeagiza vipimo sawia 750 vya kunyongeza ambavyo tunatarajiwa kuvipata
tarehe 22.5.2014
- Wizara imeweka utaratibu wa kuhakikisha vifaa
Tiba vinapatikana wakati wote katika vituo vyote kwa ajili ya kuwahudumia
wagonjwa watakaogundulika na kuwa na ugonjwa huu.
Udhibiti wa mbu na mazalia
- Kudhibiti mbu kupitia kwa kupulizia na
kunyunyizia viuatilifu katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika katika mkoa
wa Dar es salaam ambayo wametoka wagonjwa wengi wa Dengue. Hii inalenga
kuangamiza mbu wapevu na viluwiluwi.
Utafiti
Taasisi ya Utafiti ya magonjwa ya Binadamu
(NIMR) iko katika maandalizi ya kufanya utafiti kuhusu dengue
kwa kuangalia maaeneo makubwa mawili.
- Ukubwa
wa tatizo katika binadamu
- Mbu
waambukizao ugonjwa wa homa ya Dengue- kujua jamii husuka, tabia ya kuuma
watu, wapi wanapopendelea kuuma, wapi wanakozaliana kwa wingi na mazingira
yao ya kawaida.
Tafiti
hizi zinaanzia Dar es Salaam na kuhusisha wilaya zote tatu (Ilala, Kinondoni, Temeke).
Tafiti zitaendelea katika baadhi ya mikoa, ikiwa ni pamoja na mikoa 8 ambako
vituo vyetu vipo.Takwimu zitakazopatikana zitaboresha mbinu za kupambana na
ugonjwa huu
(ii)Hatua za Kudumu
- WAUJ imeandaa Mpango wa wa namna ya kukabiliana
na ugonjwa wa Homa ya Dengue. Mpango huu kwa kushirikisha sekta
mbalimbali.
- Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa wa
Dengue
Hitimisho
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa
huu kwani hauambukizwi kwa kumhudumia mgonjwa au kwa kugusa majimaji yanayotoka
kwa mgonjwa. Hata hivyo tunawashauri wananchi kwenda kwenye vituo vya afya
haraka pindi wanonapo dalili za ugonjwa huu.
Mlipuko wa Dengue unadhihirisha kuwa mazingira yetu
tunayoishi si salama. Ikumbukwe kuwa, kwa sehemu kubwa, ugonjwa huu unachochewa
na mazingira machafu. Aidha mvua hizi kubwa zinazoendelea zonachangia
kuongezeka kwa mazalio ya mbu. Utupaji, uzoaji na uhifadhi wa taka katika miji
yetu hauridhishi kiasi ambacho kinatoa fursa kwa mazalio ya mbu kuongezeka na
hata kuwa karibu zaidi ya makazi ya binadamu.
Kwa kuwa, hadi sasa hakuna chanjo wala dawa maalumu
kwa ajili ya kudhibiti au kutibu ugonjwa huu, njia kubwa ya kupambana
na ugonjwa huu ni kumzuia binadamu asimwe na mbu. Hivyo basi, mbinu
shirikishi za kutokomeza mbu inabidi zitiliwe mkazo katika mapambano dhidi ya
homa ya Dengue. Njia bora na rahisi ni kuhakikisha mazalio yote ya mbu
yanatokomezwa. Na hili laweza kufanywa na kila mtu kwa nafasi yake.Tunashauri
watu wavae nguo zinazofunika mikono na miguu na dawa zinazofukuza mbu (mosquito
repellent). Tunaelewa kuwa si kila mtu atakuwa na uwezo wa kununua dawa hizi na
ndiyo maana tunakazania swala la kuangamiza mazalia ya mbu ambalo ni jukumu
letu wote.Tunaendelea kuhamisisha watu na hasa watoto walale ndani ya vyandarua
venye viatilifu wanapolala wakati wa mchana.
Ningependa kuwakumbusha wananchi wa Tanzania kuwa, huu
ni muda muafaka wa kuzingatia utunzaji bora wa mazingira yetu. Tukitunza
mazingira yetu, nayo yatatutunza na kutuepusha na maradhi yanayoambatana na
mazingira machafu.
Charles A. Pallangyo
Katibu Mkuu
12 May 2014