Dar/Rukwa. Mkuu wa Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Moshi Chang’a aliyefariki dunia juzi atazikwa kesho Kihesa mkoani Iringa.
Chang’a alifariki juzi saa 10.15 jioni katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa tangu Machi 29,
mwaka huu kwa ugonjwa wa shinikizo la damu.Mdogo wa marehemu, Faustine Kikove alisema jana
kwamba mwili wa marehemu utasafirishwa leo saa 10.00 jioni kwa gari
kwenda Iringa.Alisema kabla ya kusafirishwa, mwili wa Chang’a
utaagwa nyumbani kwake Mbagala Kibondemaji kuanzia saa 8.00 mchana na
utazikwa kesho baada ya swala ya adhuhuri.
Akimzungumzia marehemu, alisema wakati akiwa
Kalambo, alimpigia simu akimweleza kuwa hajisikii vizuri na kwamba
alikuwa anakwenda Muhimbili kwa ajili ya kuchunguza afya yake.
“Hatukujua kwamba hali yake ingebadilika ghafla,
tulijua anakwenda kuchunguzwa afya na angerejea salama kuendelea na
majukumu ya kitaifa lakini haikuwa hivyo,” alisema .Akizungumzia kifo hicho, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya alisema ni pigo kwa Wanakalambo na mkoa mzima kwa jumla.
“Tumepoteza kiongozi ambaye alikuwa mwongoza njia
ambaye wananchi aliowaongoza walimpenda kwa ucheshi wake na uchapakazi,”
alisema.Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana
alisema katika vikao vya wakuu wa wilaya, Chang’a alikuwa mwalimu
kutokana na uzoefu wake wa kutumikia nyadhifa mbalimbali za Serikali.“Alitufundisha mambo mengi kutokana na uzoefu
wake, pia kwa sababu ni mwalimu kitaaluma na kiongozi wa muda mrefu
CCM,” alisema Rugimbana.
Nyumbani kwa marehemu viongozi walifika kutoa pole
kwa wafiwa, wakiwamo Manyanya na Rugimbana ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Saidi Meck Sadiki, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema na
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa.
No comments:
Post a Comment