Wednesday, April 9, 2014

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amechaguliwa kuwa Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amechaguliwa kuwa Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi katika Maendeleo Barani Afrika kwa mwaka 2013 .


Heshima hiyo kwa Rais Kikwete imetolewa na jarida maarufu la kimataifa la African Leadership Magazine Group na Tuzo la heshima hiyo itatolewa jioni ya kesho, Jumatano, Aprili 9, 2014, katika sherehe iliyopangwa kufanyika Hoteli ya St. Regis mjini Washington, D.C ikiwa ni pamoja na chakula cha jioni.


Tuzo hiyo itapokelewa kwa niaba ya Rais Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe, ambaye tayari amewasili mjini Washington kwa sherehe hiyo kubwa.



Tuzo hiyo ya heshima kubwa hutolewa kwa viongozi wa Afrika ambao hutoa mchango mkubwa zaidi wa kiuchumi na kijamii kila mwaka kwa watu wao na limetolewa kwa Rais Kikwete kwa mwelekeo wake usiokuwa wa kawaida na wenye mafanikio makubwa kwa masuala ya utawala bora.



Jarida hilo linasema kuwa ukweli wa hali hiyo bora ya utawala bora chini ya  uongozi wa Rais Kikwete umeendelea kumiminiwa sifa kimataifa na leo umeifanya Tanzania kuwa nchi ya kuigwa mfano kama kituo cha uhakika cha uwezeshaji kutokana na mageuzi makubwa yaliyofanywa katika sera na mifumo ya uchumi.



          Jarida hilo linasema kuwa Rais Kikwete alikuwa chaguo kubwa na la kwanza la wasomaji wa Jarida hilo ambao walipiga kura kupitia njia mbali mbali za mawasiliano za jarida hilo.



Linasema Jarida hilo, “Kuhusu maoni ya wasomaji wetu juu ya kiongozi yupi wa Afrika ambaye ni hodari zaidi kwa maendeleo ya kiuchumi na maendeleo, matokeo ya majibu ya swali hilo yamedhihirisha bila shaka yoyote kuhusu nafasi ya Rais Kikwete katika uongozi wa nchi yake. Na ushahidi uko kila mahali – ameweza kusimamia uchumi ambao umekuwa kwa wastani wa asili mia saba kwa miaka yote ya uongozi wake.”
 Sherehe za kesho, miongoni mwa mambo mengine, zitaliwezesha Jarida hilo kutangaza mafanikio ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Kikwete kwa Jumuia ya Kimataifa, ikiwa ni pamoja na Jumuia ya Kimataifa ya Kibiashara, wanadiplomasia na taasisi nyingine zenye ushawishi mkubwa katika medani za kimataifa na zenye makao yake katika Jiji la Washington na maeneo ya jirani.
         
Imetolewa na:
                                            Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,

DAR ES SALAAM.

No comments:

Post a Comment

Popular Posts