WAZIRI
MKUU PINDA JANA AMEONGOZA WATANZANIA KUAGA MWILI WA DC CHANG'A , ATAKAYE ZIKWA
LEO MJINI IRINGA
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameongoza viongozi kadhaa na
baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuuaga mwili wa aliyekuwa Mkuu wa
Wilaya ya Kalambo, Bw. Moshi Chang’a ambaye alifariki dunia Aprili 20, 2014
kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Shughuli ya kuuaga rasmi mwili wa marehemu Chang’a kwa
wakazi wa mji wa Dar es Salaam ilifanyika leo mchana (Jumanne, Aprili 22, 2014)
nyumbani kwake Mbagala, Kibonde Maji, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mwili wake utasafirishwa leo jioni kwenda Kihesa, mkoani Iringa kwa mazishi.
Akizungumza na waombolezaji hao kabla ya kutoa heshima za
mwisho, Waziri Mkuu Pinda alisema amemfahamu Bw. Chang’a kwa muda mrefu kwa
sababu sehemu kubwa ya utumishi wake ameifanya akiwa Serikalini.
“Ninyi mlimfahamu Bw. Chang’a kivingine lakini mimi
nilimfahamu kwa namna ya tofauti kutokana na jinsi alivyokuwa msaada mkubwa kwa
Serikali kila tulipokuwa tukipata shida ama migogoro ya kiuongozi.”
“Kama TAMISEMI, tumemtumia sana kusawazisha mambo kwa
sababu Mungu alimjalia kipaji cha pekee ambacho ni ucheshi... hata jambo
lingekuwa gumu vipi, huyu Bwana alijua kufikisha ujumbe bila kumuudhi mhusika
kutokana na maneno yake,” alisema Waziri Mkuu.
Alitumia fursa hiyo kufikisha salamu za rambirambi kwa
wafiwa kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko safarini kikazi.
Vilevile, aliwataka wanafamilia ambao wamebaki bila mama
wala baba, wawe na umoja na mshikamano na kuahidi kuwa Serikali itawasaidia
watoto wa marehemu wakamilishe malengo ya elimu yao kama ambavyo baba yao
alikuwa amepanga.
Marehemu Chang’a anatarajiwa kuzikwa kesho (Jumatato,
Aprili 23, 2014) huko Kihesa, Manispaa ya Iringa ambapo Serikali itawasilishwa
na Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia. Marehemu ameacha watoto
watano, wa kike watatu na wa kiume wawili.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM
JUMANNE, APRILI 22, 2014
No comments:
Post a Comment