Monday, June 23, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mjadala Bunge Maalum la Katiba halininyimi usingizi – Rais Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa hana wasiwasi na hali ya mjadala mkali uliotawala Bunge Maalum la Katiba kwa sababu ni muhimu kwa mjadala kuhusu Katiba Mpya ukawa wa kina ili kuweza kupata Katiba bora kwa Watanzania.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Katiba ya Tanzania haitapatikana kwa mikutano ya kisiasa nje ya Bunge Maalum la Katiba bali ndani ya Bunge hilo ambako ni dhahiri kuwa mjadala utatawaliwa na nguvu ya hoja na busara.
Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ametoa ufafanuzi huo mchana wa leo, Ijumaa, Juni 20, 2014, wakati alipotoa Mhadhara (Lecture) kuhusu Usalama wa Taifa (The Security of the Nation) kwenye Chuo cha Taifa cha Ulinzi – National Defence College – kilichoko Kunduchi, Dar Es salaam.
Wakati wa kipindi cha maswali na majibu, ofisa mmoja wa Jeshi la Kenya alimwuuliza Rais Kikwete kama alikuwa na wasiwasi kuhusu mjadala unaoendelea nchini kuhusu Katiba Mpya unaweza kuvuruga usalama wa Tanzania.
Rais Kikwete amemjibu: “Sina wasiwasi hata kidogo kwa sababu hatukutarajia kuwa mjadala wa Bunge Maalum la Katiba kuhusu jambo hili kubwa ungekuwa rahisi. Yalipojitokeza maoni ya Tanzania kupata Katiba Mpya, tuliunda Tume na tume hiyo ikatoa ripoti yake ambayo ndiyo inajadiliwa katika Bunge Maalum. Hatukutarajia kuwa mjadala kuhusu ripoti ungekuwa rahisi kwa wajumbe kutoa majibu ya ndiyo ama hapana.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Kinachoendelea ni jambo muhimu na la lazima…najua wakati mwingine majadiliano yalikuwa makali mno lakini hili ni jambo zuri. Aina ya mfumo na muundo wa Serikali lilizusha mjadala mkali lakini hayo ni matokeo ya hali halisi ya masuala yanayojadiliwa.”
“Ni imani yangu kuwa tutafikia mwisho. Mwisho upi, hilo ni suala la Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuamua. Muhimu ni kwamba Katiba Mpya inaweza kupatikana kutoka Bungeni tu siyo kupitia mikutano ya hadhara nje ya Bunge. Huko hakuna Katiba huko kuna mikutano ya hadhara na siasa tu. Katiba itapatikana kwa mijadala na kwa nguvu ya hoja ndani ya Bunge letu.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR ES SALAAM
20 Juni, 2014

No comments:

Post a Comment

Popular Posts