MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Jesca
Msambatavangu (39) amesema anayo nia na uwezo wa kumuangusha katika
Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini
anayemaliza muda wake Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
Msambatavangu aliyasema hayo jana ikiwa ni wiki moja tangu Makamu
Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Phillip Mangula afike mjini Iringa
kumaliza mgogoro wa kisiasa uliosababisha baadhi ya wanachama wa chama
hicho jimbo la Iringa Mjini wafukuzwe uanachama huku Mwenyekiti huyo wa
Mkoa akipewa onyo kali.
Machi mwaka huu, vikao vya chama hicho ngazi ya wilaya na mkoa
viliwafukuza uanachama Shukuru Luhambati, Clara Shirima na Hosea
Kaberege huku Msambatavangu akipewa onyo kali lililodaiwa kumuondolea
sifa ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi kupitia chama hicho na kuzusha
hofu kubwa ya mpasuko ndani yake.
Akizungumzia rufaa walizokata na maamuzi aliyokuja nayo Mangula na
kuyawasilisha katika kikao cha Halmashauri ya Wilaya ya CCM Manispaa ya
Iringa, Msambatavangu alisema; “CCM kwa kutumia kanuni na Katiba yake
imepitia rufaa zetu, ikajifunza kitu na kutumia busara yake kutupilia
mbali adhabu hizo ili kulinda maslahi mapana ya chama hiki.
“Tunajiandaa kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao tukiwa wamoja na
niwahakikishieni mimi ni mmoja kati ya wana CCM wenye nia ya kugombea
ubunge katika jimbo la Iringa Mjini.
“Sijajua makada gani wengine
watajitokeza; wenye uwezo wa kusema ni nani ni CCM wenyewe na wananchi
wa jimbo hili.
"Kwa mimi kutangaza nia na kujitoa nina hakika na ninafahamu nina
uwezo wa kupeperusha bendera na kurudi na ushindi, sitakiletea aibu
Chama Cha Mapinduzi pamoja na kwamba nipo tayari kumuunga mkono mgombea
atakayeteuliwa,” alisema.
Alitaja kipaumbele chake cha kwanza endapo CCM itampa ridhaa ya
kuwania nafasi hiyo kuwa ni elimu na katika sekta hiyo atahakikisha
miundombinu yake inaboreshwa ili iwe ya kisasa.
“Nitahakikisha kunakuwepo na ustawi wa elimu, shule bora zenye nidhamu ili Iringa iingie kwenye ushindani wa juu kitaifa.
"Tutajiimarisha kujenga mabweni katika shule zetu ili watoto hasa wa
kike wawe jirani na shule,” alisema.
No comments:
Post a Comment