Serikali ya Afrika Kusini imekana ripoti kwamba mawaziri wake walipanga njama ya kumtorosha rais wa Sudan Omar El Bashir wiki iliopita.
Katika tukio hilo nusura rais huyo akamatwe kufuatia agizo la
mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita dhidi yake kutokana na
mashtaka ya mauaji ya kimbari.
Mahakama ya Afrika Kusini ilimuagiza Bashir kusalia nchini humo huku
ikijadiliana kuhusu iwapo agizo hilo litekelezwe. Lakini kabla ya
mahakama hiyo kutoa uamuzi wake bwana Bashir aliondoka nchini Afrika
Kusini na kurudi nyumbani.
Rais huyo wa Sudan alikuwa nchini Afrika Kusini kwa mkutano wa
viongozi wa bara Afrika na kwamba serikali ilikuwa inajua kwamba
ilihitajika kumkamata kwa kuwa mwanachama wa ICC.
Kwa mujibu wa gazeti la Sunday Times nchini Afrika Kusini limenukuu
duru za serikali kwamba katika mkutano wa mawaziri ilikubalika kwamba
Afrika Kusini itamlinda hata iwapo italazimika kukiuka uamuzi wa
mahakama na kukiuka katiba.
Katika taarifa yake,serikali imekana kwamba kulikuwa na mkutano wa
siri na kwamba itaipatia mahakama hiyo maelezo kuhusu vile Bashir
alivyoondoka nchini humo.
Mahakama kuu imeipatia serikali ya taifa hilo hadi alhamisi kubaini ni vipi aliruhusiwa kuondoka.
No comments:
Post a Comment