Kutokana
na machafuko hayo, zaidi ya raia 20,000 wa Sudan Kusini, wamepoteza
maisha huku wengine zaidi ya milioni moja wakikosa makazi.
Walisaini
makubaliano hayo juzi usiku jijini Arusha, huku marais wa ndani na nje
ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wakiongozwa na
Rais Jakaya Kikwete, wakishuhudia.
Wengine
walioshuhudia makubaliano hayo ni Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Naibu
Rais wa Afrika ya Kusini, Cyril Ramaphosa , Rais wa Uganda, Yoweri
Museveni, Salva Kiir, Riek Machar na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk
Mohammed Gharib Bilal.
Kutokana
na makubaliano hayo ya kihistoria yenye lengo la kurejesha amani ya
taifa hilo changa, lililojitenga kutoka Jamhuri ya Sudan yenye makao
yake makuu Khartoum, Rais Kikwete aliwapongeza Salva Kiir, Machar na
kundi jingine la tatu ambalo baadhi ya viongozi walikamatwa na kuwekwa
kizuizini nchini humo na kuwaambia kuwa makubaliano hayo zaidi ya 40,
wahakikishe wanayazingatia ili amani na upendo vitawale nchini mwao.
Makubaliano hayo ambayo awali yalikuwa yasainiwe juzi saa 8:00 mchana, yalisainiwa saa 2:30 baada ya makubaliano rasmi.
Baadhi
ya makubaliano hayo ni pamoja na kufanyia marekebisho katiba ya chama
tawala nchini humo cha SPLM, kupunguza madaraka ya Rais, kuongeza idadi
ya wajumbe katika kamati kuu ya chama, kukubali kuwajibika wote kwa yote
yaliyotokea na kuwaomba msamaha wananchi wa Sudan Kusini kwa
kuwasababishia machafuko na vita.
Mengine
ni haki ya kila mwanachama kugombea uongozi, kuleta mabadiliko ya
kidemokrasia katika chama, utawala bora na uwazi katika chama na kutumia
makubaliano ya Arusha kuharakisha mazungumzo ya Addis Ababa (Inter
Governmental Authority Development (IGAD).
Mara
baada ya maazimio hayo kusomwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana, aliwaomba kutimiza kwa dhati maazimio waliyojiwekea na
kuyatekeleza kwa faida ya nchi yao.
Rais
Kikwete aliyeungana na marais wenzake na viongozi wengine wa kimataifa,
kushuhudia tukio la kihistoria la utiaji saini ya makubaliano ya amani
na kusitisha mapigano katika nchi mpya ya Sudan Kusini; alisema “Nawapongeza kwa hatua hii mliyofikia mlipokuja kuniomba kuwasaidia kutatua tatizo lenu la vita.
“Nilijiuliza
maswali mengi, lakini nashukuru nimeshirikiana na wenzangu wa CCM
kuhakikisha amani Sudan ya Kusini inapatikana kupitia chama, hivyo
nawasihi kuhakikisha mnasimamia haya mliyoyasaini ili kuleta maendeleo
kwa nchi sambamba na kuleta amani na furaha ndani ya nchi yenu”.
Kikwete
alisema kila kiongozi kabla ya kufanya kitu ni lazima atafakari mara
mbili jambo lolote analotaka kufanya, kuwa lina faida kwa wananchi wa
nchi hiyo au la.
“Lakini
mkiyatekeleza makubaliano haya, kila kitu kwenu kitakuwa rahisi na
hakuna litakaloshindikana kwenu na kuna usemi wa Kiswahili usemao kuzaa
si kazi, kazi kulea mwana , hivyo nawasihi mkayasimamie haya,” alisema.
Rais
Kenyatta aliwapongeza kwa kukubali kusaini makubaliano hayo na
kuwakaribisha kwake pale watakapohitaji msaada wowote kwa ajili ya
kuharakisha maendeleo ya nchi hiyo.
Kwa
upande wa Rais Museveni, aliungana na wenzake kuwapongeza kwa kufikia
hatua hiyo na kusema nchi hiyo ni ndugu wa karibu na Uganda na hivyo
imekuwa furaha kuona sasa wanakwenda kutulia bila mapigano.
“Hata
hivyo napenda kuwapongeza hawa wenzetu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa
kukubali kuratibu mazungumzo haya hadi kufikia hapa na nasema ni vyema
ukiona ndugu yako amekosea, Waswahili husema hatuwezi kuambizana ukweli
kitu ambacho kinatugharimu,” alisema.
Baada
ya hatuba hizo za wosia kwa wapinzani hao ndani ya chama kimoja, Rais
Salva Kiir na mpinzani wake, Riek Machar ambaye ndiye aliyekuwa Makamu
wa Rais kabla ya mtafaruku, walionekana wenye furaha muda wote na
kupongezana kwa kupeana mikono mara kwa mara, huku wakishangiliwa na
wapambe wao waliofurika ndani ya ukumbi wa Ngurudoto, jijini Arusha.
Wapinzani
hao wote kwa pamoja waliahidi kutimiza kwa vitendo makubaliano hayo na
kupeana ushirikiano katika mambo yote na kuwashukuru wote waliohusika
kusuluhisha ugomvi huo hadi kufikia hatua hiyo.
Alikuwepo
pia Rebecca Nyandeng De Mabior, mjane wa kiongozi wa kwanza wa chama
cha SPLM, John Garang, ambaye ndiye aliyeongoza harakati za kupigania
uhuru, kuelekea kujitenga kwa nchi hiyo, kutoka kwa iliyokuwa Jamhuri ya
Sudan.
Mazungumzo
ya awali ya vikundi vinavyozozana katika chama cha SPLM yaliongozwa na
ujumbe mzito wa ngazi ya juu wa CCM ili kutafuta suluhu ya mgogoro ndani
ya chama hicho, kinachotawala nchini Sudan Kusini.
Ujumbe
huo uliongozwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Malecela
aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania,
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula na Kinana.
Kwa upande wa SPLM, mazungumzo hayo yaliongozwa na Taban Deng Gai, Daniel Awet Akot, na Deng Alor Kuol.
Miongoni
mwa makundi hayo ni kutoka chama cha SPLM, kundi kutoka kwa wafungwa wa
kisiasa, pamoja na kundi lililojitenga kutoka chama cha SPLM.
Chama
hicho kiligawanyika makundi matatu na kusababisha jeshi kwa upande
wake, kumeguka katika makundi hayo na kusababisha wananchi nao
kugawanyika katika makundi hayo matatu .
Mazungumzo
hayo pia yalihudhuriwa na wawakilishi kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Umoja
wa Afrika (AU), Norway, Misri, Umoja wa Mataifa (UN) na Ethiopia.
No comments:
Post a Comment