Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Rehema Nchimbi
amewataka viongozi mkoani hapa na Iringa kuacha tabia ya kudai nyongeza
wanaponunua mazao ya wakulima kwa sababu hiyo ni lumbesa.
Nchimbi alisema hayo jana katika mkutano wa wadau
kutoka sekta ya umma na binafsi wa utekelezaji wa Sheria ya Mizani na
Vipimo ya mwaka 1982.
“Nawaomba viongozi mbadilike kitabia, tuko hapa
kuipiga vita lumbesa kwa sababu ni uvunjani wa sheria pia inatuharibia
miundombinu ya barabara vijijini kutokana na uzito kuzidi. Lakini
madhara yake mengine ni kumnyonya mkulima,” alisema Nchimbi.
Aliwataka wakulima na wafanyabiashara kuzinduka dhidi ya vipimo batili kwa kuunda kikosi kazi kitakachopambana na hali hiyo.
“Wanunuzi nao wana tabia ya kuomba kila kitu iwe
sukari, chumvi na wakati mwingine hata nyama kwa sababu hawataki kutumia
vipimo halali,” alisema Nchimbi.
Katibu Mtendaji Chama cha Wafanyabiashara wenye
Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Iringa, James Sizya alisema wameunda
kikosi kazi kwa ajili ya kutekeleza sheria hiyo.
Alisema kikosi hicho kinajumuisha maofisa kilimo, biashara, polisi na wakulima.
Sizya alisema vita hiyo inatakiwa kuamshwa kwa kutoa elimu ili kufanikiwa.
Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Iringa, Lucas
Mwakabungu alisema: “Muswada wa marekebisho ya sheria hiyo ulioandaliwa
mwaka 2013 unapendekeza adhabu iongezwe kwa kuwa faini ya sasa ni
Sh100,000 ni ndogo,” alisema Mwakabungu.
No comments:
Post a Comment