WAZIRI
Mkuu, Mizengo Pinda ameagiza watendaji katika Manispaa na Jiji
waliohusika kunyang’anya mali za wafanyabiashara mbalimbali kwa
kisingizio cha kusafisha jiji na kugawana badala ya kupeleka
kunakoruhusiwa kuchukuliwa hatua huku akiahidi kumshughulikia Katibu
Tarafa wa Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
Aidha,
amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kukaa na wafanyabiashara na
kuangalia njia nzuri ya kufanya biashara ili kuondoa vurugu baina yao na
vijana.
Pinda
aliyasema hayo jana wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa
Waziri Mkuu alipojibu swali la Mbunge wa Ilala, Iddi Zungu (CCM)
aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu wanamgambo wanaotumia nafasi ya
kusafisha jiji kuwanyanyasa wafanyabiashara na kugawana mali zao huku
tatizo kubwa likiwa kwa Katibu Tarafa wa Kariakoo.
Amesema
yeye binafsi alitumiwa picha ya watendaji hao wakigawana mali
walizowanyang’anya wafanyabiashara wakiwamo mama lishe, jambo ambalo ni
kuwanyanyasa na kuwarudisha nyuma kimaendeleo.
Waziri Mkuu alikemea kitendo cha watendaji wa jiji na mikoa kutumia kusafisha jiji kunyanyasa wananchi.
Hivyo
aliagiza wakuu wa wilaya na mikoa kukaa na wafanyabiashara ndogo na
kupanga jinsi ya kuendesha biashara kistaarabu ikiwa ni pamoja na
kupanga masoko ya jioni na Jumapili ili wafanye biashara muda mfupi na
kuondoka.
No comments:
Post a Comment