Wednesday, January 28, 2015

PROFESA LIPUMBA AKAMATWA NA POLISI KWA NGUVU! TAARIFA KAMILI.



Ndugu zangu, hivi punde nimeongea na Maharagande Mbarala na Bonifasia Mapunda na wamenijulisha kuwa, Profesa Lipumba na Manaibu Wakurugenzi wawili wa Chama Cha Wananchi CUF (Shaweji Mketo na Abdul Kambaya), pamoja na walinzi wa Profesa Lipumba, wamekamatwa na polisi. Pia, nimeongea na mhe. Joram Bashange, Mkurugenzi wa Fedha wa CUF, tayari yuko Central Police lakini hajaruhusiwa kuwaona viongozi. Mawakili wa CUF wanaelekea polisi pia.


KUMBUKIZI YA MWAKA 2001

Ukamataji huo uliotumia nguvu kubwa umetokea leo majira ya Mchana wilayani Temeke. Leo ni Januari 27 na ni siku yenye kumbukumbu muhimu kwa Chama Cha Wananchi CUF baada ya matukio ya mauaji yaliyofanyika tarehe na mwezi kama huu huko Zanzibar ambako wafuasi wa CUF zaidi ya 100 waliuawa kwa risasi na vyombo vya dola. Mauaji hayo yalifuatiwa na maandamano mbalimbali yakiwemo ya Dar Es Salaam yaliyoongozwa na Prof. Lipumba ambaye alivunjwa mkono, kuporwa saa yake ya thamani na polisi, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.

MAANDAMANO YA CUF KILA MWAKA:

Baada ya tukio hilo CUF imekuwa na utaratibu wa kuandamana kila mwaka (maandamano ya amani) ili kuwakumbuka wahanga wa mauaji ya Januari 2001 na kuwaenzi waliopata ulemavu wa kudumu kutokana na kipigo cha vyombo vya dola. Mwaka jana 2014 mwezi kama huu Bendera za Chama cha Wananchi CUF zilipepea nusu mlingoti na pia maandamano yalifanywa maeneo kadhaa ya nchi na vyombo vya dola viliyalinda.

Mwaka huu nimeambiwa kuwa CUF ililijulisha jeshi la polisi juu ya maandamano ya leo kupitia barua ya Alhamisi, Tarehe 22 Januari 2014. Baada ya CUF kuandika barua hiyo, maandalizi ya maandamano na mkutano wa hadhara yaliendelea, ikiwemo kufanya matangazo kwenye wilaya za DSM, kukodi vifaa mbalimbali na hata kulipia matangazo LIVE kwenye redio kadhaa ili hotuba za viongozi ziweze kurushwa. Jeshi la polisi lilipokea barua hiyo tokea tarehe 22 Januari na likakaa kimya muda wote huo.

ZUIO LA POLISI:

Leo tarehe 27 Januari, maandamano yalipangwa kuanza saa 8 mchana kuanzia Temeke Mwisho kwenda hadi viwanja vya MBAGALA ZAKIEM ambako mkutano wa hadhara ungefanyika kuanzia saa 10.00 - 12.00 jioni. Cha ajabu ni kuwa, asubuhi ya leo ndipo Jeshi la Polisi limepeleka barua kwenye Ofisi Kuu za CUF Buguruni KUZUIA MAANDAMANO na MKUTANO WA HADHARA.

Barua hiyo iliyosainiwa na Kaimu Kamishna wa Polisi Kanda ya Dar Es Salaam na Pwani inaeleza sababu kadhaa za zuio hilo:
1. Kwamba, maandamano ya CUF ya Mwezi Januari 2001 yaliyofanya vyombo vya dola vitumie nguvu na kuua raia hayakuwa halali na hivyo kuadhimisha siku hiyo mwaka huu ni haramu na kunaweza kuhatarisha amani ya nchi.
2. Kwamba, Taarifa za kiintelijensia zinaonesha ati kuna watu wamepanga kufanya vurugu katika maandamano na mkutano huo.
3. Kwamba, kuna vitisho vya UGAIDI katika nchi yetu na hivyo maandamano hayo na mkutano huo vinaweza kuleta madhara ya magaidi kupenya na kutekeleza azma zao mbaya.
4. Sababu nyingine za kipuuzi, dhaifu na zisizo na maana.
Baada ya kupokea barua hiyo na kwa sababu wananchi na wapenzi wa CUF walikwishajikusanya kwa maelfu kwa ajili ya maandamano, ilimpasa Profesa Lipumba na viongozi waandamizi wa chama waweze kwenda hadi Temeke Mwisho ili kuahirisha maandamano hayo.

TEMEKE MWISHO:

Majira ya mchana leo, Profesa Lipumba aliongea na wanachama na wapenzi wa CUF waliojazana Temeke Mwisho karibu na Ofisi za CUF Wilaya na akaahirisha maandamano na mkutano (Usalama wa Taifa walikuwepo, Polisi walikuwepo kwa mamia na vyombo vya habari vilikuwepo). Baada ya kufanikiwa kuwatawanya wafuasi waliokuwa Temeke Mwisho, Profesa akajulishwa kuwa kule uwanjani Zakiem tayari kuna maelfu ya wafuasi, ikampasa yeye na viongozi waandamizi waingie katika magari na kuanza safari kwenda Zakiem kwa lengo la kuwatawanya wafuasi kwa amani kama alivyofanya kwa wale waliokusanyika Temeke Mwisho. Hapakuwa na wafuasi wa chama waliomfuata.

KUELEKEA MBAGALA ZAKIEM:

Wakiwa katika Magari yao na katika safari ya kwenda Mbagala Zakiem, wakazuiwa na magari zaidi ya 10 ya polisi walio tayari kwa mapambano. Profesa na viongozi wakawajulisha Polisi azma yao ya kwenda kutawanya wafuasi walioko Zakiem, baada ya mvutano mfupi Polisi hao waliwaruhusu waende Zakiem. Safari ya magari machache ikaendelea, bila wafuasi wanaotembea kwa miguu.

Walipofika mbele (Mtoni Mtongani - Round about) wakakuta BLOCK ya pili ya mamia ya Polisi wenye magari na silaha. Hawa nao wakawazuia wasiende ZAKIEM, wakati bado Profesa anawaelewesha, mabomu yakaanza kupigwa na viongozi kusambaratishwa kwa nguvu mno kama vile kulikuwa na jambo kubwa. Profesa amebebwa mzobemzobe akipigwa virungu na kutupwa kwenye DIFENDA ya polisi yeye, wakurugenzi wake na walinzi wake. Hivi sasa tuongeavyo wako CENTRAL POLICE na mie nilitoka tu kidogo Darasani ili kupiga simu na kusimuliwa tukio zima.

 
 
CHA KUSHANGAZA:

Wakati polisi wanazuia maandamano ya CUF kwa nguvu kubwa kiasi hiki, wanawapiga na kuwajeruhi viongozi wasio na hatia na ambao wamejishusha na kuahirisha maandamano na mkutano wao, Polisi haohao kila siku tunaona wanasimamia maandamano na mikutano ya Mwigulu Nchemba, Abdulrahman Kinana, Nape Nauye na viongozi chungu mbovu wa CCM.

Hata katika maadhimisho ya miaka 38 ya CCM yanayotarajiwa kufanyika mkoani Ruvuma, nimejulishwa kuwa kuna maandamano yamepangwa yakihusisha wana CCM mbalimbali katika wilaya za jirani ili kusheherekea sikukuu yao na kwamba Polisi watayalinda maandamano hayo ya CCM.


MASWALI YA KUJIULIZA:

Je, hizi taarifa za Kiintelijensia zinafanya kazi kwa mikutano na maandamano ya vyama vya upinzani tu? Je, hao Magaidi wao wanavamia na kulipua mikutano ya vyama vya upinzani tu? Magaidi gani hawa ambao hawaendi kuvamia wezi wa fedha za umma ati wanakwenda kuvamia viongozi waadilifu wanaopigania haki sawa kwa wote na mabadiliko makubwa katika nchi yetu? Tunadhani matendo haya ya serikali na vyombo vyake dhidi ya vyama vya upinzani yanajenga mustakabali wa taifa? Yanajenga amani na upendo miongoni mwetu? Au yanazidisha chuki na uhasama na mgawanyiko/mpasuko katika taifa?

Kwa nini mamia ya askari wanaokwenda kupiga na kujeruhi viongozi wenye nia njema yasitumike kwenda kusaka majambazi walioua askari wetu pale Ikwiriri Rufiji? Kwa nini mamia ya askari hao yasiwasake majambazi walioteka mabasi ya abiria mkoani Arusha majuzi? Kwa nini mamia ya Askari hao yasijielekeze kuwasaka wauaji wa Albino na wazee wenye macho mekundu Shinyanga?

Kwa nini mamia ya askari hao wasipelekwe kuwasaka magaidi ambao tumegundua watakuja kutuvamia? Na mbona maguvu hayo ya polisi yasielekezwe kuwasaka wala rushwa wakubwa, wafadhili na wamiliki wa mitandao ya kuuza madawa ya kulevya, wezi wa fedha za umma na waharibifu wakuu wa Taifa hili?
Mbona taifa hili linaendeshwa kipuuzi namna hii? Mbona nchi yetu inapelekwa mbele kama vile kuwa Chama Cha Upinzani ni dhambi dhidi ya watawala wezi na mafisadi? Kwa nini basi CCM hao hao wakapigia debe kuanzishwe vyama vingi mwaka 1992? Sasa wanaogopa na kuweweseka kwa lipi?

(UKIONA SERIKALI INAOGOPA MAANDAMANO YA AMANI NA MKUTANO WA CHAMA KIMOJA TU HADI KUPIGA NA KUKAMATA VIONGOZI, JUA KWAMBA SERIKALI HIYO HAINA SIKU NYINGI MADARAKANI).

"Time will determine and judge each of us".


Julius Mtatiro,
27 Januari 2015,
Masomoni.

No comments:

Post a Comment

Popular Posts