HALI inazidi kuwa tete kwa vigogo kadhaa wa Serikali juu ya sakata la
uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow,
baada ya kuwapo taarifa kuwa wengi watafikishwa mahakamani.
Iwapo leo vigogo ambao majina yao yamekuwa yakitajwa tangu juzi
watafikishwa mahakamani, wataongeza idadi baada ya juzi watumishi wawili
wa Serikali kufikishwa katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Jana asubuhi baadhi ya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), walionekana wakiranda katika viwanja vya mahakama
hiyo.
Mmoja wa maofisa hao alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya kuwapo
kwao eneo hilo, alisema wapo kwenye maandalizi ya kuwapandisha kizimbani
vigogo wengine.
Hata hivyo, ilipotimu saa 7 za mchana, ofisa huyo alisema kuna baadhi ya
nyaraka za watuhumiwa zilikuwa zinarekebishwa kabla ya kufika
mahakamani.
Baadhi ya watuhumiwa ambao jana walipigiwa simu na kutakiwa kufika
Takukuru, inaelezwa hawakupokea simu kwa hofu ya kuburuzwa mahakamani.
Hadi tunakwenda mitamboni harakati hizo zilikuwa zimekwama.
Watumishi waliofikishwa mahakamani juzi ni Mkurugenzi wa Huduma za
Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa
Majunangoma ambaye alisomewa mashtaka ya kupokea rushwa ya Sh milioni
323.4 zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow kutoka kwa Mkurugenzi
wa Kampuni ya VIP Engeering James Rugemalila.
Kabla ya Rugonzibwa kufanya kazi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, alikuwa mwanasheria wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(RITA), ambako alihusika na mufilisi wa Kampuni ya IPTL.
Rugonzibwa, aliichunguza IPTL, alisimamia watumishi wake wakati kampuni
hiyo iko katika mufilisi na alisimamia mashauri mbalimbali yanayoihusu.
Mshitakiwa mwingine, ni Theophillo Bwakea ambaye alifikishwa mahakamani
kwa kosa la kupokea rushwa ya Sh milioni 161.7 kutoka kwa Rugemalila.
Bwakea
ni Mhandisi Mkuu wa Mradi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA), na kabla
ya kufanya kazi huko, alikuwa Wizara ya Nishati na Madini, kitengo
cha kusimamia umeme, ambako anadaiwa alishiriki kutunga sera ya kampuni
binafsi kuuza umeme Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na ilipoanza
kutumika, Kampuni ya kufua umeme ya IPTL ilikuwa ya kwanza kupata
zabuni.
Ngeleja agoma
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria
na Utawala, William Ngeleja, amewagomea wajumbe wa kamati hiyo
waliomtaka ajiuzulu kutokana na kutajwa kuhusika na mgawo wa fedha za
Escrow.
Pamoja na hatua hiyo, wajumbe walimtaka Ngeleja ajizulu au akae pembeni
ili kumpisha makamu mwenyekiti aongoze vikao jambo ambalo alilipinga.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mnadhimu
wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ambaye ni mjumbe kwenye kamati
hiyo, alisema tangu kuanza kwa vikao hivyo Januari 13, mwaka huu,
Ngeleja amekuwa akiviendesha kwa nguvu licha ya wajumbe kumtaka akae
pambeni.
“Amekuwa akiendesha vikao tangu juzi na hata juzi aliendesha na kuondoka
saa 4 na kumwachia makamu wa kamati hii kumshikia,” alisema.
Alisema juzi baada ya Ngeleja kukaa na kuanza kuendesha kikao hicho,
alimtaka kuachia kiti hicho kama ambavyo maazimio manane ya Bunge
yalivyowataka wenyeviti waliotajwa kuhusika katika kashfa hiyo ya Tegeta
Escrow ambapo yeye anadaiwa kupewa mgawo wa Sh bilioni 40.4 kinyume na
sheria.
Lissu alisema pamoja na kumshauri kuachia ngazi, bado Ngeleja aligoma
kwa madai akifanya hivyo ataonyesha wazi kuwa alihusika katika kashfa
hiyo.
“Ngeleja alisahau katika azimio la Bunge, halikusema wale waliotuhumiwa
walikuwa wezi, lakini akashindwa kujua katika azimio jingine Bunge
lilitaka vyombo vya uchunguzi kuchunguza ili watakaobainika wachukuliwe
hatua ambazo zitathibitisha kama walihusika au la,” alisema Lissu.
Alisema sheria ya maadili ya uongozi wa umma, inawataka viongozi wa umma
kutojihusisha na migongano ya kimaslahi na vitendo vya rushwa.
“Kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma, Ngeleja baada ya kutajwa
katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
akihusishwa kupokea fedha hizo, ilitosha atangaze kujiuzulu,” alisema
Lissu.
Alisema kama Ngeleja, ataendelea kukiuka uamuzi wa Bunge, suala hilo watalirudisha bungeni ili lijadiliwe upya.
Zitto
Akizungumzia kuhusu suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, alimsihi Ngeleja kutekeleza
maamuzi ya Bunge kwa kuachia nafasi hiyo.
“Namsihi Ngeleja kama kijana mwenzangu atekeleze maamuzi ya Bunge na aache kumtega Spika Anne Makinda,” alisema.
SOURCE MPEKUZI
No comments:
Post a Comment