TAASISI ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, imepinga tamko la
maaskofu kuhusu kuzuia kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na kusema hatua
hiyo ni sawa na kuingilia uhuru wa Bunge.
Kutokana na hali hiyo, wametaka maaskofu hao kupitia Jukwaa la Wakristo
Tanzania (TCF), kuwaacha wabunge ili waweze kujadili muswada huo kwa
uhuru bila kuwapo shinikizo katika suala hilo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa taasisi hiyo,
Sheikh Khamis Mataka, alisema tamko lililotolewa na maaskofu ni sawa na
kuingilia madaraka ya Bunge na kutaka kuifanya Serikali ichukiwe kwa
kuonekana imeshindwa kutimiza ahadi iliyoitoa kupitia Waziri Mkuu
Mizengo Pinda.
“Tamko lililotolewa na maaskofu halina hoja, hawana sababu za msingi za
kuikataa Mahakama ya Kadhi, tunawasihi na kuwaomba maaskofu waachie
uhuru wa wabunge hasa waumini wa dini ya Kikristo walioko bungeni, ili
waweze kuujadili muswada huo bila shinikizo la kiimani.
“Mbinu zozote za kuwashawishi wabunge kiimani kutekeleza maazimio ya
maaskofu chini ya Jukwaa la Wakristo Tanzania zitaleta udini na jaribio
la kuligawa Bunge kiimani, jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa
taifa letu,” alisema Sheikh Mataka.
Alisema wabunge wanapaswa kuzingatia viapo vyao vya kuwatumikia wananchi
kwa uadilifu bila kuathiriwa na shinikizo la kiimani lililotolewa na
maaskofu.
Sheikh Mataka alisema taasisi inawakumbusha maaskofu kwamba Serikali ina
vyombo vya uchunguzi na utafiti vyenye uwezo wa kubaini maeneo
yanayovunja umoja wa kitaifa pamoja na mambo yanayokwenda kinyume na
Katiba ya nchi ambapo wao si sehemu ya vyombo hivyo.
Alisema hofu ya kuwapo kwa Mahakama ya Kadhi bara ni bandia kwa kuwa
kesi za Kiislamu zinazohusu masuala ya talaka, mirathi, wosia, wakfu na
malezi ya watoto zinaamuliwa kwa sheria na taratibu za dini hiyo.
“Wanachoomba Waislamu ni kubadilishwa hakimu na kuondoa malalamiko na
uonevu, hasa kwa wanawake ambapo lengo ni kuwapo mtu anayejua sheria na
kuamua kuamua kesi hizo,” alisema.
Sheikh Mataka, ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya
Bakwata Taifa, alisema migogoro ya kiimani ya ndani, hasa kwa Waislamu
isitumike kama kigezo cha kupinga mahakama hiyo kwa upande wa Tanzania
Bara.
Alisema Mahakama ya Kadhi haihusiani na migogoro ya Wakristo, bali ni
kuamua masuala ya Waislamu, huku akishangazwa na hatua ya maaskofu hao
kupinga mchakato huo hali ya kuwa hauwahusu na wala haugusi imani yao.
“Tutashangaa iwapo Serikali itaamua kuuondoa bungeni muswada unaolenga
kuitambua Mahakama ya Kadhi kwa kuitungia sheria maalumu. Je, iweje leo
kuwa na maneno ya kila aina ya kushinikiza kuondolewa kwa muswada huo,
hili hapana, wabunge waachwe waamue kwa utashi wao na sio kuingiliwa na
makundi ya nje,” alisema.
Sheikh Mataka alisema kama Mahakama ya Kadhi ingekuwa na matatizo, ni
wazi isingeanzishwa kwa upande wa Zanzibar ambako hadi sasa imekuwa
ikitumika pasi na kuwapo na migogoro ya aina yoyote.
Juzi, viongozi wengine wa dini ya Kiislamu walipinga tamko lililotolewa
na Jukwaa la Wakristo kuhusu sheria hiyo ya kuanzishwa Mahakama ya Kadhi
na kudai kuwa matamko ya aina hiyo yanaweza kusababisha machafuko
nchini.
Kauli hiyo zimekuja baada ya Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) kutoa
waraka juzi, likipinga muswada unaopendekeza kuanzishwa Mahakama ya
Kadhi unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni wakati wowote.
Kutokana na hali hiyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju,
aliwatoa hofu Wakristo wanaohofia mpango wa Serikali wa kuitambua
kisheria Mahakama ya Kadhi nchini.
Alisema pamoja na kwamba mpango huo umeanza kulalamikiwa na baadhi ya
makundi ya kidini, nia hiyo haina madhara kwa wananchi kwa kuwa Serikali
haiwezi kupitisha sheria itakayowagawa watu.
SOURCE MPEKUZI
No comments:
Post a Comment