Sitasahau siku niliyokimbiwa na mume wangu baada ya kumzalia
pacha kwa mara ya tatu mfululizo.” Hii ni kauli ya Salome Paul Mhando,
mama wa watoto sita ambao ni pacha, aliowazaa kwa nyakati tofauti katika
kipindi cha miaka sita iliyopita, wakipishana miaka miwili miwili.
Salome, alitelekezwa nyumbani na mumewe huyo baada
ya kujifungua pacha kwa mara ya tatu, huku wakiwa hawana sehemu maalumu
ya kuishi, achilia mbali njaa iliyotokana na umaskini wa kipato.
Baada ya kutelekezwa, msamaria mwema alijitolea
kumhifadhi katika shamba lake lililopo eneo la Mabwepande nje kidogo ya
Jiji la Dar es Salaam, kabla ya kupata msaada wa nyumba ya kuishi.
Mama huyo anayekumbuka tukio hilo kwa uchungu,
anasimulia kuwa mumewe aliyemtaja kwa jina moja la Ali, alimtoroka saa
saba mchana na kumwacha akiwa na pacha hao.
Anabainisha kuwa tukio hilo lilitokea baada ya familia hiyo kukaa na njaa kwa siku kadhaa kutokana na umaskini wa kipato.
“Siku hiyo, ambayo tarehe yake siikumbuki, mume
wangu alirudi nyumbani akiwa tena hana chakula na kunieleza kuwa
anaumwa. Nilipomwuuliza sasa tunafanyaje kuhusu chakula, alitoka nje,”
anaeleza mama huyo na kuendelea:
“Nikaamua kumfuata na kuanza kumsema nikimdai
chakula. Baadaye (mumewe) akaniuliza mbona unanisema? Mimi nikamjibu;
naulizia masuala ya chakula, tunafanyaje leo? Akasema; basi niache
naenda kukitafuta.”
Salome anaeleza kuwa kinyume na ahadi hiyo, tangu
wakati huo alipoondoka hajaonekana nyumbani hadi sasa. “Niliamua kwenda
kulala, lakini nikiwa na wasiwasi kuhusu usalama wake. Nikapatwa na hofu
nikijiuliza; nini kimempata mwenzangu na kuanza kuwapigia simu ndugu
zake ambao pia hawakupatikana.”
Salome anasema jitihada za kuwatafuta ndugu wa
mumewe ziligonga mwamba na hadi sasa hana mawasiliano yoyote na familia
hiyo ya mumewe.
Anaeleza kuwa kutokana na mumewe huyo kutorudi
tena nyumbani, alilazimika kwenda kwenye vyombo vya habari kuomba msaada
wa malezi ya watoto hao.
“Nilikwenda kwanza ITV ambako mbali na kunisaidia
katika mahitaji ya msingi ya chakula, walinitangaza pia kwenye luninga
kuwa ninahitaji msaada na tukio hilo ndilo limenisaidia kupata msaada wa
kudumu.
Hali ikoje?
Salome anahusisha kutoroka nyumbani kwa mumewe na ugumu wa maisha unaoikabili familia hiyo.
“Nina watoto pacha sita; wawili wana umri wa miaka
sita, wawili wengine wana umri wa miaka minne na wawili wa mwisho wana
umri wa miezi 12. Nasikitika kukimbiwa na mume kwa sababu ya ugumu wa
maisha, lakini zaidi akidai kuwa ninazaa sana. Maisha ni magumu na
ninashukuru kwa misaada ninayoendelea kuipata kutoka kwa jamii, hasa
kupatiwa msaada wa nyumba ya kuishi na wanangu,” anasema.
Akifafanua kuhusu ugumu wa maisha, Salome anasema
ameshindwa hata kuwapeleka shule watoto wake wakubwa... “Hakuna
anayesoma, wote bado wako nyumbani.”
Msaada wa nyumba
Hata hivyo, ugumu wa maisha wa Salome umeigusa
Benki ya Covenant ya jijini Dar es Salaam, ambayo imejitokeza kumnunulia
nyumba ya kuishi na watoto hao eneo la Mabwepande.
Mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Sabetha
Mwambenja anasema mbali na msaada huo, anatamani kuona mume huyo
aliyemtelekeza anapatikana na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Anasema benki yake ilitambua mahitaji ya mama huyo
kupitia vyombo vya habari na kuamua kumpa msaada wa kumnunulia nyumba
ya kuishi yenye thamani ya Sh25 milioni, ambayo alikabidhiwa juzi.
“Tumemkabidhi, nyumba, tukamnunulia magodoro,
vitanda vinne, mashuka na taa za sola na familia nzima tumeikatia bima
ya afya itakayowawezesha kutibiwa katika hospitali yoyote inayotoa
huduma kupitia bima hiyo,” anaeleza mkurugenzi huyo.
“Sisi hatuna kitengo wala idara inayojishughulisha
na matatizo ya jamii, tumeguswa tu na tatizo la mama huyo aliyekimbiwa
na mumewe sababu ya kumzalia pacha. Natoa wito kwa benki nyingine na
wadau mbalimbali wa maendeleo kuguswa na matatizo ya jamii
inayowazunguka na kusaidia pale inapowezekana,” anasema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo,
Balozi Salome Sijanona anasema baada ya kuona mateso aliyokuwa akiyapata
mwanamke huyo kwa kukosa makazi, chakula na mahitaji mengine ya
kibinaadamu, waliona ni vyema kujitolea kumsaidia ikiwa ni moja ya
kutimiza majukumu yake kwa jamii.
“Tumeguswa na mateso aliyokuwa akipata Salome Mhando, yeye
pamoja na watoto wake, baada ya kutelekezwa na mumewe kwa kigezo ha
kuzaa watoto pacha mfululizo. Tuliguswa na kuamua kujitolea kumnunulia
nyumba ambayo ataimiliki mwenyewe,” anasema Balozi Sijaona na kuongeza:
“Nyumba hii tumemkabidhi pamoja na samani za ndani
ambazo sasa zitamwezesha kuishi maisha ya amani na furaha akiwa kama
wanawake wengine na kufurahi pamoja na watoto wake.”
Shukrani
“Ninaishukuru Benki ya Covenant kuniwezesha
kumiliki nyumba yangu, ninawashukuru na ninaomba waendelee na moyo huo
wa kuwasaidia kina mama wenye matatizo kama haya kwa sababu siko peke
yangu,” alisema Salome na kuongeza:
“Kina mama tumekuwa na wakati mgumu katika ndoa
zetu hususan katika masuala ya uzazi. Ninawashukuru watu wote ambao
walijitolea kunisaidia chakula na nguo katika wakati wote nilipokuwa
sina sehemu maalumu ya kukaa, hadi sasa ninamiliki nyumba yangu.”
SOURCE MWANANCHI
SOURCE MWANANCHI
No comments:
Post a Comment