Baada ya kufanikisha lengo la kuonana na familia zaidi ya 30 za
Watanzania waliofungwa katika magereza mbalimbali Hong Kong, Padri wa
Kanisa Katoliki, John Wootherspoon aliyeleta ujumbe wa watu hao amesema
anatamani kuonana na Rais Jakaya Kikwete ili amweleze hali ya biashara
ya dawa za kulevya na manung’uniko ya wafungwa hao.
“Nilichoona
ni kuwa Tanzania imetawaliwa na rushwa, vijana wengi wanaingia katika
dawa za kulevya kwa sababu ya umaskini. Umaskini wenyewe naona kuwa
kiini chake ni rushwa. Natamani nizungumze naye iwapo atakubali,”
alisema Padri Wootherspoon.
Akizungumza na gazeti la Mwananchi, Wootherspoon, raia wa Australia na padri wa parokia ya
Notre Dame, Shing Tak Street, Hong Kong, Kowloon, anasema anatamani
azungumze na Rais Kikwete ili amweleze hali halisi ya biashara ya dawa
za kulevya kwani kukutana kwake na wafungwa wa Kitanzania mjini Hong
Kong kumempa fursa ya kujua mengi.
Katika ziara yake ya
hapa nchini ya kutembelea familia za wafungwa hao wa dawa za kulevya
kwenye magereza ya Hong Kong, Macau na Guang Zhou, Padri Wootherspoon
pia alionana na kamishna wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya,
Godfrey Nzowa.
Kadhalika Wootherspoon alisema kati ya
mengi aliyonayo, anatamani kumwambia Rais afanye kila liwezekanalo ili
kuhakikisha Watanzania hao wanarudishwa nchini kama Nigeria
ilivyofanikiwa.
“Hata kitengo cha Haki za Binadamu cha
Umoja wa Mataifa kinaeleza wazi kuwa, mfungwa ana haki ya kuhukumiwa
katika nchi yake. Lakini nashangaa kuona kwa nini suala hili limekuwa
gumu kufanikiwa hapa,” alisema.
Akihutubia taifa katika
sherehe za kilele cha mbio za Mwenge mwaka jana mkoani Tabora, Rais
Kikwete alisema serikali imefanya jitihada mbalimbali za kukabiliana na
uingizwaji wa dawa hizo, hali aliyosema imesaidia kuwakata wasafirishaji
wanaotumia njia mbalimbali kusafirisha dawa hizo.
Wootherspoon alisema anaamini kuwa Rais Kikwete ni mkarimu,
mwelewa na amejaribu kulivalia njuga suala hili la dawa za kulevya,
lakini imekuwa vigumu kwake kufanikisha kutokana na mazingira.
“Nia
yangu kubwa ni kuwafanya vijana wasiende tena nchi za mashariki ya
mbali. Huko kuna hatari ya kunyongwa, si kuzuri. Wasikubali pia kutumiwa
na hawa wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya. Ombi langu ni
kutaka waache kufanya biashara hiyo,” alisisitiza.
Tatizo bado kubwa
Wafungwa
hao ambao wengi wanatumikia kifungo cha maisha na wengine kati ya miaka
20 hadi 25, wanalalamika kuwa matajiri wanaowatuma hawachukuliwi hatua
za kisheria, licha ya wao kuwataja kwa majina na kuweka wazi ushahidi
kwa viongozi wa Serikali wanaowatembelea magerezani, China.
Hata
hivyo, Nzowa alisema kuwa tayari magwiji wa dawa za kulevya waliokuwa
wanaipa serikali wakati mgumu, wameshatiwa nguvuni na kilichobaki ni
hukumu tu.
Bila ya kuwataja vigogo hao, Kamishna Nzowa
anasema kesi zao tayari zimeshafikishwa mahakamani na kuwa wengi
walishikwa na vithibiti, hali inayofanya kesi zao kuwa nyepesi
kukamilika.
"Tulifanya kila tuwezalo tukawamata magwiji
wenyewe, ambao wanawatumia vijana kubeba dawa hizo. Kwa sasa asilimia
kubwa tayari tumewakamata lakini bado kazi haijamalizika kama
tunavyodhani. Huu mtandao ni mkubwa,” alisema.
No comments:
Post a Comment